Na LEONARD ONYANGO
MOJA ya mambo makuu ambayo huenda yakasababisha ugonjwa wa corona kuendelea kuwepo humu nchini kwa muda mrefu si mapuuza ya kanuni zilizowekwa na wizara ya Afya kupunguza maambukizi – bali ni habari feki za kupotosha kuhusu chanjo ya corona.
Tangu Kenya kuanza kutoa chanjo ya AstraZeneca wiki iliyopita, mitandao ya kijamii imefurika kwa madai ya kupotosha ambayo huenda yakatatiza juhudi za serikali kutaka kupunguza maambukizi.
Waatalamu wa wanatabiri kuwa Kenya itakuwa imeshinda corona iwapo angalau Wakenya milioni 37, ambao ni sawa na asilimia 80 ya idadi ya watu nchini, watapewa chanjo.
Siku moja baada ya dozi milioni 1 za chanjo ya AstraZeneca kuwasili humu nchini Jumanne wiki iliyopita, Chama cha Madaktari wa Kanisa Katoliki humu nchini wakiongozwa na Dkt Stephen Karanja waliwataka Wakenya kutumia njia mbadala za kupambana na maradhi ya corona badala ya kukimbilia kupewa chanjo.
“Chanjo si lazima, kuna njia mbadala za kupambana na virusi vya corona kama vile kujifukiza (kupiga chungu) angalau mara mbili kwa siku unapohisi dalili za ugonjwa wa corona. Kadhalika mwathiriwa anaweza kupewa tembe za Ivermectin au Hydroxychloroquine,” wakadai madaktari hao.
Kutia msumari moto kwenye kidonda, madaktari hao walidai kuwa chanjo ya corona huenda ikasababisha watu kushindwa kupata watoto katika siku za usoni.
“Chanjo ya AstraZeneca imetengenezwa kwa kutumia chembechembe za figo ya binadamu ambazo zimefanyiwa ukarabati wa kisayansi, maarufu GMO, ili kufanana na virusi vya SARS-Cov-2 ambavyo husababisha ugonjwa wa corona. Chembechembe hizo hufanya mwili kutoa kinga thabiti ambazo hupigana na virusi vya corona vinapoingia mwilini,” wakasema madaktari kupitia barua yao waliyoandika Machi 3, 2021.
Matabibu hao wa Kanisa Katoliki pia walidai kuwa chanjo za Pfizer na Moderna ambazo tayari zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO), zinaharibu vinasaba vya mwili (DNA) na vinaweza kusababisha mwili kugeuka GMO.
“Ukivuna pamba au mahindi ya GMO na kisha uchukue mbegu zake na kupanda tena haziwezi zikamea. Hiyo inamaanisha kuwa chanjo za corona zinaweza kusababisha miili yetu kuwa ya GMO hivyo watoto watakaozaliwa na watu waliochanjwa wanaweza kushindwa kuzaa katika siku za usoni,” wakadai madaktari hao.
Baadhi ya Wakenya wamekuwa wakieneza madai ya kupotosha kwamba hatua ya viongozi wakuu serikalini kukosa kupewa chanjo, ni ishara kuwa wanatilia shaka usalama wake.
Kaimu Mkurugenzi Mkuu wa Huduma za Matibabu Dkt Patrick Amoth, alikuwa mtu wa kwanza humu nchini kupewa chanjo hiyo.
“Acha ningoje miaka mitano, ikiwa Dkt Amoth atakuwa buheri wa afya ndipo nitakubali kupewa chanjo hiyo,” akasema John Bundi kupitia mtandao wa Facebook.
“Tangu janga la virusi vya corona lilipoanza, Mungu amekuwa akinilinda na sioni haja ya kupewa chanjo,” akadai Mark Mutinda kupitia Twitter.
“Hii chanjo ni ya watu ambao tayari wamemaliza kuzaa, sitaki kukosa watoto,” akasema Linda Mukami kupitia Facebook.
Lakini Dkt Githinji Gitahi, Afisa Mkuu Mtendaji wa Amref Afrika, amepuuzilia mbali madai hayo ya Chama cha Madaktari wa Kanisa Katoliki huku akisema kuwa hayana mashiko kwani si msimamo wa kanisa hilo.
Kulingana na Dkt Gitahi, taarifa hiyo ilitolewa na kundi la madaktari wenye itikadi kali ambao wamekuwa wakipinga aina mbalimbali za chanjo, ikiwemo chanjo ileya kuzuia kupooza au Polio.
“Huo si msimamo wa Kanisa Katoliki bali ni maoni ya kundi la madaktari wenye itikadi kali ambao wamekuwa wakipinga chanjo kama vile ya polio na tetekuwanga (tetanus),” anasema Dkt Githinji.
Askofu wa Kanisa Katoliki wa Dayosisi ya Nyeri Anthony Muheria, pia alipuuzilia mbali ushauri huo wa madaktari wa kanisa hilo akisema kuwa wanalenga kupotosha Wakenya.
“Kanisa linaunga mkono chanjo ya kupambana na virusi vya corona. Tunahitaji kukabiliana na janga hili kwa kukubali kupewa chanjo,” akasema Askofu Muheria.
Kiongozi wa Kanisa Katoliki Papa Francis na mtangulizi wake Benedict XVI walidungwa chanjo hiyo miezi miwili iliyopita.
Watu wote – mapadri, wanahabari na wafanyakazi wa ndege – walioandamana na Papa Francis katika ziara yake ya siku tano iliyomalizika jana nchini Iraq walichanjwa kabla ya kuondoka Vatican.
Katika mahojiano na runinga moja ya nchini Italia, Papa Francis alisema; “Ninaamini kwamba kila mtu anastahili kudungwa chanjo. Ni wajibu wako kulinda maisha yako na maisha ya watu wengine.”
AstraZeneca ni miongoni mwa chanjo za corona ambazo tayari zimeidhinishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) baada ya kuthibitisha ubora wake.
AstraZeneca pia imeidhinishwa na Mamlaka ya Kutathmini Ubora wa Dawa ya Ulaya (EMA).
EMA ilipendekeza kuwa chanjo ya AstraZeneca itolewe kwa watu wa kuanzia umri wa miaka 18 na zaidi.
Shirika la WHO linasema kuwa chanjo zote zilizoidhinishwa kutumika ni salama kwa afya na wala haziharibu DNA kama inavyodaiwa.
“Teknolojia iliyotumika kutengeneza chanjo za corona za Pfizer na Moderna, kwa mfano, zimekuwepo kwa zaidi ya miaka kumi sasa. Teknolojia hiyo ndiyo ilitumika katika kutengeneza chanjo ya maradhi ya Zika, virusi vinavyotokana na kichaa cha mbwa kati ya maradhi mengineyo,” linasema.
“Kwa kawaida DNA inapatikana ndani ya kitovu (nyuklia) cha seli. Chanjo ya corona huingia ndani ya seli lakini haina uwezo wa kufika ndani ya nyuklia hivyo haiwezi kudhuru DNA,” likaongezea.
Uzazi
Shirika la WHO limepuuzilia mbali madai kwamba chanjo ya corona inasababisha wanawake kushindwa kupata ujauzito.
“Kufikia sasa hakuna ushahidi wowote kwamba chanjo za corona zinasababisha wanawake kushindwa kupata ujauzito.
“Wanawake 23 walioshiriki katika majaribio ya chanjo ya Pfizer mwaka jana kwa mfano, baadaye walikuwa wajawazito na walijifungua salama. Hakukuwa na kisa chochote cha mimba kuharibika,” linasema WHO.
Madai kwamba chanjo ya corona inasababisha wanawake kushindwa kupata ujauzito yalianzishwa na mwanasiasa mmoja wa nchini Ujerumani aliyedai kuwa inashambulia kitovu kinachounganisha mtoto aliye tumboni na mama (Umbilical cord).
Mwansiasa huyo Wolfgang Wodarg, ambaye aliachana na utabibu 1994, alisema kuwa kampuni zilizotengeneza chanjo ziliharakisha kwa lengo la kujitajirisha.
Mnamo Desemba, Wodarg aliandikia barua Mamlaka ya Kudhibiti Dawa ya Ulaya (EMA) akiitaka kusitisha kuidhinishwa kwa chanjo iliyotengenezwa na kampuni ya Pfizer-BioNTech.
“Chanjo hiyo inaweza kushambulia protini aina ya syncytin-1 ambayo huusika pakubwa katika kutengeneza kitovu cha mtoto anapokuwa tumboni. Ukosefu wa kitovu kunamaanisha kuwa mimba zitakuwa zinaharibika,” akadai.
Baadaye, uchunguzi uliofanywa miongoni mwa wanawake 40,000 ulibaini kuwa madai ya mwanasiasa huyo yalikuwa ya kupotosha.
Wajawazito
Shirika hilo la Umoja wa Mataifa (UN), linasema kuwa japo chanjo ya AstraZeneca iliyoko nchini Kenya haikufanyiwa majaribio miongoni mwa wanawake wajawazito, ingali salama.
“Chanjo ya AstraZeneca haikufanyiwa majaribio kwa wajawazito hivyo hakuna ushahidi wowote wa kuonyesha kuwa si salama kwao. Lakini wanaweza kupewa chanjo hiyo ikiwa watakuwa kwenye hatari kubwa ya kuambukizwa corona,” linashauri WHO.
Aidha shirika hilo linasema chanjo ya AstraZeneca, iliyo na uwezo wa kuzuia virusi vya corona kwa asilimia 63, haifai kupewa watu wa chini ya umri wa miaka 18.
Waziri wa Afya Mutahi Kagwe, hata hivyo, ametangaza kuwa chanjo hiyo haitatolewa kwa wanawake wajawazito na wale wanaonyonyesha.
Changamoto za chanjo
Chanjo ya AstraZeneca imekuwa ikikumbana na changamoto tele tangu ilipoanza kutumika kukabiliana na maambukizi ya virusi vya corona.
Mnamo Jumapili wiki jana, Austria ilisitisha shughuli ya kutoa chanjo ya AstraZeneca baada ya mtu mmoja kufariki ghafla na mwingine kuugua baada ya kupewa chanjo hiyo.
Idara ya kusimamia usalama wa matibabu (BASG) ilisema kuwa ilipokea ripoti kuhusiana na madhara ya chanjo hiyo katika kiniki ya Zwettl iliyoko katika mkoa wa Lower Austria.
Serikali, hata hivyo, ilisema kuwa hakuna ushahidi kwamba kifo cha mwanamume huyo wa umri wa miaka 49 kilisababishwa na chanjo hiyo.
Korea Kusini tayari inaendelea na uchunguzi kuthibitisha kiini cha vifo vya watu wawili walioaga dunia siku chache baada ya kudungwa chanjo ya AstraZeneca wiki iliyopita.
Wizara ya afya ya nchi hiyo, hata hivyo ilisema waathiriwa waliokuwa na zaidi ya umri wa miaka 60, walikuwa wakiugua magonjwa mengine kama vile maradhi ya moyo.
Vile vile, mtu anayepokea chanjo ya AstraZeneca hupatwa na matatizo ya kiafya ya muda mfupi kama vile, mwili kuhisi unyonge, uchovu, baridi, maumivu ya kichwa, kichefuchefu na maumivu ya vifundo vya mikono na miguu.
Mnamo Januari, Norway ilisitisha kwa muda chanjo ya Pfizer baada ya wazee 23 kufariki pindi baada ya kupewa kinga hiyo.
Lakini baadaye, serikali iliruhusu chanjo hiyo iendelee kutumika baada ya kubaini kuwa wazee hao walikuwa na matatizo mengineyo ya kiafya.
Serikali ilishauri wahudumu wa afya wasitoe chanjo hiyo kwa wazee walio na magonjwa mengineyo.
Chanjo ya Moderna pia imebainika kuwa inasababisha eneo lililodungwa kufura kwa zaidi ya siku 10.
Article first published on https://taifaleo.nation.co.ke/?p=72358