AMREF inavyosaidia mapambano ya UKIMWI Simiyu

by Amref Health Africa

*Asilimia 83 wanaoishi na VVU wanajua hali zao

*Idadi ya wanaojitokeza kupima VVU nayo yaongezeka

Na Derick Milton, Busega

Mkoa wa Simiyu kwa kushirikiana na Shirika la AMREF Health Africa kupitia mradi wake wa Afya Kamilifu, umefanikiwa kuwafikia asilimia 83 ya watu wote ambao wanaishi na virusi vya UKIMWI na wanatambua hali zao.

Kiwango hicho ambacho ni chini ya kiwango cha Kitaifa ambacho ni asilimia 89, kimetajwa kuongeza kwa kasi kubwa ndani ya mwaka mmoja tangu kuanza kutekelezwa kwa mradi huo wa Afya Kamilifu.

Hayo yamebainishwa Januari 29, 2022 na Mratibu wa Kudhibiti UKIMWI Mkoa wa Simiyu, Dk. Khamis Kulemba, wakati wa kikao kazi cha tathimini ya kuangalia mwenendo wa shughuli za kupambana na Virusi vya UKIMWI mkoani humo.

Amesema licha ya mafanikio hayo, bado changamoto kubwa ipo kwa vijana pamoja na wanaume, ambao idadi yao imekuwa ndogo katika kujitokeza kupima afya zao kulingana na makundi mengine.

“Mkoa wa Simiyu kupitia mradi wa Afya kamilifu unaotekelezwa na kwa mwaka mmoja umefanikiwa kufikia asilimia 83 ya watu wanaoishi na Virus Vya UKIMWI kutoka asilimia 76 ikiwa ni moja ya malengo mapya ya Programu ya Pamoja ya Umoja wa Mataifa kuhusu VVU yenye dhumuni la kumaliza janga hilo ifikapo mwaka 2030,” amesema Dk. Kulemba.

Amesema kuwa wanaume ambao wametambua Afya zao ni asilimia 70 huku vijana wakiwa asilimia 50 hadi 60, hali ambayo ameeleza kuwa wamejiwekea mikakati mizito yenye lengo la kuhakikisha wanawafikia kwa kiwango kikubwa zaidi.

“Vijana wenye umri wa kuanzia miaka 15 hadi 19, lakini pia wanaume kuanzia miaka 19 hadi 25, kundi hili bado lipo nyuma sana katika kupima afya zao, tumejadili na kuweka mikaka mipya ya kuhakikisha tunawafikia wengi zaidi katika kipindi kifupi,” amesema Dk. Kulemba.

Hata hivyo amelipongeza shirika la Amref kupitia mradi wa afya kamilifu, kwani umekua na tija kubwa katika kufikia malengo hayo ya 95 tatu kwani ndani ya mwaka mmoja wa utekelezaji wa mradi wa Afya Kamilifu wamefikia asilimia 83 ya wenye VVU kujua hali zao.

“Ukifanikisha kuwapima wenye VVU na wakajua hali zao, inarahisha kutekeleza afua nyingine ya 95 ya wanaojua hali zao kuanzishiwa matibabu lakini pia kurahisisha 95 ya walioko kwenye matibabu kufubaza makali ya VVU,” amesema Dk. Kulemba.

Aidha, ameeleza kuwa katika kikao hicho, wamejadili juu ya mapambano ya ugonjwa wa Uviko-19, ambapo wameweka mikakati kuongeza nguvu katika kampeni ya wananchi kupata chanjo kwa kila Halmashauri kuhakikisha kila siku inachanja watu 500.

Meneja wa Mradi wa Afya Kamilifu Mkoa wa Simiyu, Mathias Abuya, amesema AMREF kupitia mradi huo katika mapambano dhidi ya UKIMWI wamekuwa wakishirikiana na serikali kwa kuboresha upatikanaji wa huduma za upimaji, tiba na matunzo kwa watu wenye VVU.

Amesema AMREF kupitia mradi huo imekuwa ikisaidia katika eneo la rasilimali watu kwa kuajiri wataalamu wa afya na kuwakabidhi serikalini ili kupunguza changamoto ya uhaba wa watumishi inayoikabili sekta ya afya.

Amesema mradi huo unatekelezwa na AMREF Health Africa kwa kushirikiana na Tanzania Communications Development Centre (TCDC) na University of Maryland Baltimore (UMB) na kwamba unaunga mkono malengo mapya ya Programu ya pamoja ya Umoja wa Mataifa kuhusu VVU naUKIMWI ya 95-95-95, ambapo lengo ni kupanua tiba ya kufubaza virusi ili kumaliza janga la UKIMWI ifikapo 2030.

Mratibu Takwimu za Afya Mkoa wa Simiyu, Godfrey Justine amesema shirika la AMREF limesaidia sana kuongeza wingi wa watu kujitokeza kupima VVU.

“Ukiangalia kwa kiwango kikubwa mabadiliko yametokea, wingi wa watu kujitokeza kupima VVU umeongezeka, lakini pia waliogunduliwa kuwa na maambukizi wameingizwa katika huduma za dawa, tiba na matunza,” amesema Justine.

Naye Mganga Mkuu wa Wilaya ya Busega, Dk. Godfrey Mbangali amesema kupitia mradi huo kwenye wilaya hiyo AAMREF wamefanikisha kuongeza Vvituo vya kutoa huduma kwa watu wenye VVU (CTC) kutoka 12 hadi 16.

Article first published on https://newsafricanow.com/tanzania/amref-inavyosaidia-mapambano-ya-ukimwi-simiyu/

You may also like

Leave a Comment

* By using this form you agree with the storage and handling of your data by this website.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

This website uses cookies to improve your experience. We'll assume you're ok with this, but you can opt-out if you wish. Accept Read More