Dar es Salaam. Shirika la Kimataifa la utafiti wa tiba na afya barani Afrika (Amref) limesema litaendelea kutoa hamasa na kuhakikisha kina mama wanapata huduma bora za afya wakati wa ujauzito hadi kujifungua.
Juzi shirika hilo kwa kushirikiana na Benki ya Azania (ABL), Kupitia kampeni yake ya ‘Stand up for African Mothers’ (SU4AM) jana lilifanya matembezi ya hisani yaliyohusisha viongozi wa Serikali na wananchi ili kukusanya Sh1 bilioni zitakazosaidia upatikanaji wa wakunga katika vituo vya afya nchini.
Akizungumza katika viwanja vya Green Grounds, Oysterbay jijini hapa mara baada ya matembezi Mkurugenzi mkazi wa Amref Dk Florence Temu alisema uwepo wa wakunga wenye utaalamu katika vituo vya afya utapunguza au kuepusha vifo vinavyotokea wakati wa kujifungua.
“Wakunga ni kiungo muhimu katika kutoa huduma stahiki za afya hasa ya uzazi wakati wa kujifungua na baada ya kujifungua. Tunaomba na kuwasihi wananchi wote, mashirika, kampuni binafsi na washirika wa maendeleo, kuendelee kuchangia ili kufanikisha hili la kuokoa maisha ya mama na mtoto katika maeneo yenye uhitaji,” alisema.
Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa ABL, Charles Itembe , alisema benki hiyo kusaidia sekta ya afya, hasa katika afya ya uzazi ni moja ya nguzo za msingi za sera ya uwajibikaji wa kijamii.
“Wanawake ni nguzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi, bila ya huduma bora za afya na za msingi, wanawake katika nchi zinazoendelea kama Tanzania wataendelea kupotea maisha kwa vifo vya uzazi hali itakayosababisha kuzorota kwa maendeleo,” alisema Itembe.
Article first published on https://www.mwananchi.co.tz/habari/Kitaifa/Amref-yasisitiza-uwepo-wa-wakunga-kila-kituo-cha-afya/1597296-5177268-hu4agz/index.html