Vijana Wahimizwa Wajitokeze Kwa Wingi Kupata Chanjo

by Amref Health Africa

NA LAWRENCE ONGARO

IDARA ya afya ya umma inalenga kuwapa chanjo vijana ambao kwa kawaida ndio wengi kwa idadi katika Kaunti ya Kiambu.

Mkurugenzi wa afya ya umma Bi Teresa Kariuki, alieleza kuwa hata ingawa wamepiga hatua kwa kuchanja wakazi wa Kiambu bado idadi kubwa ya vijana wanastahili kupata chanjo hiyo dhidi ya Covid-19.

Alisema kwa wakati huu wanalenga kufikia asilimia 40 ya vijana ambao wengi wao hawajapokea chanjo hiyo.

“Kwa muda mrefu kumekuwa na changamoto kwa vijana kujitolea wenyewe kwenda kuchanjwa hospitalini, na kwa hivyo tunatafuta njia mwafaka ya kuwafikia,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Mkutano huo pia ulifadhiliwa na shirika la masuala ya afya la AMREF.

Aliyasema hayo mnamo Alhamisi eneo la Juja katika hafla iliyojumuisha washika dau wapatao 60 kutoka sekta mbalimbali.

Alieleza kuwa ilikuwa ni muhimu kufanya mkutano huo ili kuelewa changamoto zinazopatikana katika sekta hizo kuhusiana na maswala ya chanjo dhidi ya Covid-19.

Baadhi ya walioshiriki kwenye hafla hiyo walieleza dhana tofauti zinazosambazwa kwa wananchi kuwa inadhuru miili ya watu kwa njia moja ama nyingine.

Kulingana na takwimu ulitolewa na idara ya afya ya umma, katika kaunti ya Kiambu watu wapatao 1,124,753 milioni tayari wamepata chanjo ya Covid-19 ilipofika mwezi Disemba 2021.

Hata hivyo kufikia wakati huo pia watu wapatao 2,650 walikuwa wameambukizwa na homa ya Covid-19.

Hiyo ni kama asilimia 41.4 kwa wanaume na 58.7 kwa wanawake.

Kulingana na mkurugenzi huyo, wamezindua mbinu mpya watakayotumia ili kuwashawishi vijana waweze kupokea chanjo dhidi ya Covid-19.

Alisema watasajili vijana wenzao ili kuwarai kuchanjwa katika makanisa, na hata viwanjani wanakoshiriki michezo mbalimbali.

Alieleza pia watatumia mitandao, na burudani za muziki ili kuwaleta karibu vijana hao.

“Tumejaribu kwa muda mfupi na tumepata matokeo ya kuridhisha kwa kuwaleta karibu vijana hao,” alifafanua mkurugenzi huyo.

Katika hafla hiyo waandishi wa habari pia walihimizwa kuwa mstari wa mbele kuangazia yote yanayotendeka kuhusiana na janga la Covid-19 ili wananchi waelewe ukweli wa mambo.

“Tunaelewa vyema ya kwamba waandishi wa habari wana jukumu kubwa la kuangazia mengi kuhusu maswala ya covid-19 ili kila mwananchi aelewe umuhimu wa kuchanjwa,” alieleza mkurugenzi huyo.

Alisema hata ingawa kuenea kwa homa ya Covid-19 kunaendelea kupungua, lakini ni vyema watu kuendelea kuwa makini na kujichunga kwa kufuata maagizo yote ya idara husika za afya “ili tukabiliane nayo ipasavyo.”

Article first published on https://taifaleo.nation.co.ke/covid-19-vijana-wahimizwa-wajitokeze-kwa-wingi-kupata-chanjo/

You may also like

Leave a Comment

* By using this form you agree with the storage and handling of your data by this website.

This site uses Akismet to reduce spam. Learn how your comment data is processed.

This website uses cookies to improve your experience. We'll assume you're ok with this, but you can opt-out if you wish. Accept Read More